Na Faustin Kamugisha
“MUWE TAYARI siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari
za tumaini lililo
ndani yenu” (1 Pet 3: 15). Kuna aliyekuwa anagonga
jiwe kwa nyundo ili alivunje vipande vipande. Aligonga mara mia moja
jiwe halikunjika akakata tamaa.
Mwenzake waliyekuwa wanafanya kazi hiyo pamoja alikuja na kugonga
jiwe mara moja jiwe lilivunjika. Ilihitajika mara ya mia na moja jiwe
livunjike lakini mgongaji wa kwanza alikata tamaa. Kukata tamaa ni
mwisho wa matumaini. Mtume Petro anatutaka tuitikie wito huu: “Muwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu” (1 Pet 3: 15).
Tumaini lililo ndani yetu ni hili: Maisha pamoja na Yesu ni
matumaini yasiyo na mwisho, bila yeye, ni mwisho usio na matumaini.
Tumaini letu ni hili: “Sitawaacha ninyi yatima” (Yn 14: 15-21). “Matumaini hayamuui yeyote.” Hii ni methali ya Kongo. Ingawa matumaini hayaliwi kama chakula hatuwezi kuishi bila matumaini. “Matumaini ni nguzo ya dunia.” Ndivyo
isemavyo methali ya Kiafrika. Matumaini ni kumpokea Roho Mtakatifu.
“Nao wakampokea Roho Mtakatifu” (Mdo 8: 17). Kukata tamaa ni kumkataa
Roho Mtakatifu.
Matumaini ni mtazamo chanya
Watu wanapokwambia, “Kata tamaa,” matumaini yanasema, “jaribu tena.”
Watu wanapokwambia, “nusu glasi haikujaa,” matumaini yanasema, “nusu
glasi imejaa.” Watu wanapokwambia, “matatizo ni mengi,” matumaini
yanasema, “yana mwisho” Watu wanapokwambia, “mlango wa kazi umefungwa,”
matumaini yanasema, “Mungu anafungua mlango mwingine.”
Siku moja nilikutana na msichana niliyesoma naye Chuo Kikuu. Alikuwa
na mimba. Aliniambia Mungu amemfungulia mlango, dirisha na madirisha
madogo. Niliuliza namna gani aliniambia kuwa baada ya kumaliza masomo
chuo kikuu alipata kazi. Pili alimpata mume bora. Tatu alikuwa na mimba.
Mungu wetu si kuwa anaweza kukufungulia mlango tu bali anaweza
kukufungulia milango na madirisha. Endelea kuvumilia na endelea kuamini
ukitafuta suluhisho la shida. Endelea kutumaini.
Matumaini ni silaha
Shetani alitumia mateso, misiba, balaa, na mikosi kumkatisha Ayubu
tamaa. Lakini ayubu hakukata tamaa. “Hapo shetani akaondoka mbele ya
Mwenyezi Mungu, akamtesa Ayubu…Mkewe akamwambia, ‘Bado tu ungali
ukishikilia unyofu wako? Mtukane Mungu, ufe?
Ayubu akamjibu mkewe, “…Tukipokea mema kutoka kwa Mungu, kwa nini
tukatae kutoka pia mabaya kutoka kwake?” (Ayubu 2: 7-10). Ayubu alitumia
silaha ya matumaini kwa Mungu katika mapambano yake na shetani.
Matumaini yamebeba uvumilivu. Mvumilivu hula mbivu. Kupata pancha sio
mwisho wa safari. Matumaini yamebeba subira. Subira yavuta heri.
Yesu ni shujaa wa matumaini
Maisha pamoja na Yesu ni matumaini yasiyo na mwisho, bila yeye, ni mwisho usio na matumaini.
Yesu alipokuwa msalabani alivumilia sababu alikuwa na matumaini katika
ufufuko na katika ushindi. Makuhani wakuu, waandishi, na wazee
walimcheka wakisema, “Aliwaokoa wengine, kujiokoa mwenyewe hawezi.
Kama ni mfalme wa Israeli, basi ashuke sasa msalabani, nasi
tutamsadiki” (Mathayo 27: 42). Yesu hakushuka toka msalabani. Ni kama
unamwambia askari atoke uwanja wa vita ili umwamini kuwa ni askari. Ni
kama unamwambia mwanandoa atoke kwenye ndoa ili umwamini kuwa ameolewa.
Ni kama unamwambia mwanafunzi aache shule ili umwamini kuwa yeye ni
mwanafunzi. Yesu hakushuka toka msalabani alivumilia. Matunda yake ni
kwamba kwa uvumilivu wake alituonyesha njia. Hakuna Jumapili ya Pasaka
bila Ijumaa Kuu. Alitukumboa. Fikiria stampu kwenye barua. Manufaa
yake yapo katika uwezo wake wa kubaki kwenye bahasha mpaka bahasha
imfikie mlengwa. Huo ni mfano wa nguvu ya uvumilivu wa kulishughulia jambo kwa muda mrefu bila kuliacha.
Matumaini ni hitaji la binadamu
Matumaini yetu yawe kama nywele na kucha. Haijalishi unazikata mara
ngapi haziachi kuota. Hata ukiwa kwenye matatizo kuwa na matumaini.
Matatizo ni giza la kukusaidia kuona nyota. Katika giza la matatizo
uwe na matumaini. Ukitembea usiku wenye giza unaona nyota. Katika
mtazamo huo Stephanie Meyer alisema: “Napenda usiku Bila giza
tusingeona nyota.”
Katika matatizo unahitaji kuwa na matumaini. Usikatishwe tamaa na
giza la maneno ya kukukatisha tamaa. Baba wa Uchimbaji mafuta Edwin L.
Drake aliambiwa mwaka 1859: “Unataka kuchimba mafuta? Unamaanisha
kuchimba ardhi ukitafuta mafuta utakuwa umerukwa na akili!” Kilichofuata
ni historia bwana huyo hakusikiliza maneno ya kukatisha tamaa. Katika
yote unahitaji matumaini. Ni kweli alivyosema Louise Phillipe: “Giza
linapokuwa giza nene, nyota inaangaza sana.”
Biblia yasema: “Kabila lililotembea gizani limeona nuru kuu” (Isaya
9:2). Katika kutembea gizani unaweza kuona nyota. Wana wa Israel
waliogandamizwa na kuteswa katika giza la mateso waliona nuru kuu.
“Nyakati za balaa mbaya sana na machafuko zimekuwa nyakati za
uzalishaji kwa watu wanaofikiri sana. Chuma kisichokuwa na uchafu
kinatolewa penye joto jingi sana. Radi inayoangaza sana inatokana na
wingu na dhoruba jeusi sana,” alisema Charles Caleb Colton.
Kumbe matatizo ni giza la kusaidia kuona nyota. Vitu vingi
vimevumbuliwa kutokana na matatizo. Waisraeli katika matatizo makubwa ya
ukame wamegundua kilimo cha umwagiaji kwenye shina la mche tu.
Wanazalisha matunda na kuuza nchi za nje nchi yenye ukame.
Katika matatizo ya giza umeme umevumbuliwa. Tulizoea kusema barua ni
nusu ya kuonana. Katika matatizo ya kutoonana sasa kumevumbuliwa namna
ya kuonana kupitia Skype. Sio vizuri kuwa na matatizo ukabweteka.
Pengine si vizuri sana kungojea giza ili uone mwanga. Methali ya
Kifaransa inasema: “Yeye anayengojea kuvaa viatu vya marehemu anaweza kutembea pekupeku kwa muda mrefu.”
Katika matatizo makubwa tunaweza kutambua uwepo wa Mwenyezi Mungu.
Tunaweza kumwona Mungu. Biblia yasema: “Usifurahi juu yangu, ewe adui
yangu, maana nikianguka, nitasimama tena, nikikaa katika giza, Bwana ni
mwangaza wangu” (Mika 7:8).
Katika giza utamwona Bwana mwangaza wako. Matatizo uliyonayo ni
mwaliko wa kuwa na matumaini. Geuza hasi iwe chanya. Badili sumu iwe
dawa. Badili jangwa liwe msitu. Badili mlima uwe tambarare. Penye giza
washa mshumaa. Penye chuki panda upendo. Katika mto usiopitika jenga
daraja.
Matumaini yawe mtaji wako na raslimali yako kwamba inawezekana.
Matumaini yatakuletea furaha katika giza la matatizo. “Kwa
tumaini,mkifurahi katika dhiki, mkisubiri” (Warumi 12:12). Matumaini
yetu yaendane na hali halisi yasionekane kama kichekesho. Kuna mpangaji
aliyeulizwa: “Lini utalipa malimbikizo ya kodi ya chumba?” Alijibu:
“Muda mfupi baada ya kupokea cheki ambayo mchapishaji wa kitabu changu
atanipa nitakulipa.
Hii itategemea kama atakubali kuchapisha kitabu hicho ambacho
napanga kuandika nitakapapata jambo la kuandika juu yake na wazo
fulani.” Ndoto zifanyiwe kazi. Kama una ndoto ya kujenga ghorofa angani
anza kujenga msingi kuanzia chini. “Si kwamba mambo ni magumu ndio maana
hatuthubutu, ni kwa sababu hatuthubutu ndiyo maana mambo ni magumu,”
alisema mwanafalsafa Seneca.
“Namna tunavyoona tatizo ni tatizo,” alisema Stephen R. Covey.
Unaweza kuona tatizo ni giza tu. Namna hiyo ya kuona ni tatizo. Lakini
unaweza kuona tatizo kama giza la kukusaidia kuona nyota. Kumbe tatizo
si tatizo. Tatizo ni namna tunavyoliona tatizo.
Nchi zilizoendelea zimekabiliana na matatizo makubwa kwa mtazamo
ambao si tatizo. Tunaweza kusema matatizo makubwa maendeleo “makubwa”.
Mateso mengi na neema nyingi. Kumbuka kuwa penye matatizo kuna neema.
Penye hasi kuna chanya. Penye kivuli kuna mwanga. Painamapo ndipo
painukapo.
Usikate tamaa pancha sio mwisho wa safari
La kuvunda halina ubani. Maji yakimwagika hayazoeleki. Ni methali za
kukatisha tamaa. Methali hizi zina maana kuwa jambo likiharibika
haliwezi kurekebishwa. Harufu mbaya ya uozo wa tabia haizuiwi.
Kwa shetani la kuvunda halina ubani. Kwa Mungu la kuvunda lina ubani.
Kwa shetani maji yakimwagika hayazoeleki, kwa Mungu maji yakimwagika
yanazoeleka. “Hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu.” (Luka 1: 37) Mbinu
ya nne ambayo shetani huitumia kuwafanya watu washindwe kutenda mazuri
wengine wajiue ni kukata tamaa.
Shetani alitumia mbinu hii ya kukata tamaa kwa Yuda Iskarioti ambaye
alimuuza Yesu baadaye Yuda Iskarioti alijiua. Tunasoma hivi katika
Biblia, “Shetani akamwingia Yuda aitwaye Iskarioti…akaenda, akajadiliana
na makuhani wakuu na walinzi wa hekalu kuhusu atakavyomsaliti Yesu
kwao.” (Luka 22: 2-4) Maandiko haya yanasema shetani alimuingia Yuda.
Shetani alitumia mbinu yake ya kukata tamaa. “Yuda…alipoona kwamba
wamekwisha mhukumu Yesu…akazitupa zile pesa hekaluni, akatoka nje,
akaenda akajinyonga.” (Mathayo 27: 3-5) Yuda Iskarioti aliona kuwa
mipango yake imeharibika alikata tamaa.
Tatizo la dhambi ni kuwa mtu anaweza kuchukia hata zile pesa ambazo
hakupata kwa njia ya halali. Yuda alichukia zile pesa. Kama Yuda
Iskarioti angeomba msamaha tungekuwa na historia nyingine labda ya
Mtakatifu Yuda Iskarioti Msimamizi wa Benki, Msimamizi wa watunza pesa
na Msimamizi wa Taasisi za Pesa. Alikata tamaa na kukosa matumaini ya
kusamehewa.
Kuna methali ya wamasai isemayo, “Matumaini sio sawa na kukuta
tamaa.” Mtu ambaye amekata tamaa hamlilii Mungu. Yuda hakumlilia Mungu.
Mtu aliyekata tamaa hatafuti na haombi msamaha. Maisha yakikosa malengo
yanakosa na maana. Namna hiyo sababu ya kuishi inaweza kuponyoka toka
mikononi mwa mtu. Matumaini ni kinyume cha kukata tamaa.
Mwandishi wa makala haya ni Padri wa Jimbo Katoliki Bukoba 0763-612246
No comments:
Post a Comment