Mungu
alichokuwekea hakiozi. Ni methali ya Tanzania. Ni methali ambayo inatia
matumaini kwa watafutaji na waliokata tamaa. Makubwa Mungu aliyokuwekea
yatafunuliwa mbele kwa mbele. Utukufu ni mbele kwa mbele. Mungu anaweza
kubadili miiba ikawa maua, anaweza kubadili hasi ikawa chanya, anaweza kubadili
machozi ya huzuni yakawa machozi ya furaha. Katika nyufa za maisha Mungu
anaweza kuleta mwanga wa matumaini. Mwandishi wa nyimbo Leonard Cohen aliandika, “Kuna nyufa katika
kila kitu; hivyo ndivyo mwanga unavyoingia.” Kioo cha mbele cha gari ni kikubwa
kuonesha kuwa makubwa yako mbele. Vioo vya upandeni vya kutazama ya nyuma ni
vidogo kuonesha kuwa madogo yako nyuma, utukufu ni mbele kwa mbele. Yesu
alipogeuka sura mlimani alitaka kuwaonesha mitume wake utukufu ni mbele kwa
mbele.
Mitume wa Yesu
wamekata tamaa Yesu alipowaambia atasulubiwa msalabani. Katika maisha yao
palikuwepo na ufa wa kukata tamaa. Yesu alipogeuka sura mlimani mwanga wa
matumaini uliingia katika nyufa zao za kukata tamaa. Petro alimwambia Yesu,
“Mwalimu, ni vizuri kwetu kukaa hapa; tutajenga vibanda vitatu, kimoja chako,
kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya.” (Luka 9: 33). Petro hakujua kuwa utukufu ni
mbele kwa mbele. “Petro
hakulielewa bado neno hilo alipotamani kuishi na Kristo mlimani. Amekuwekea
hayo, Petro, baada ya kifo chako lakini sasa yeye mwenyewe anakuambia: shuka
kuangaika duniani, ukatumikie duniani, ukadharauliwe, ukasulubiwe duniani.Uzima
umeshuka ili kuuawa:Njia imeshuka ili isikie uchovu wa duniani; chemichemi
imeshuka ili kupata kiu;nawe wakataa kuteseka? “ (Mt. Augustino Sermo 78,6: PL38,492-493;Lk9:33). Mtaka cha uvunguni
sharti ainame. Utukufu utakaopatikana mbele kwa mbele lazima kuufanyia kazi.
Yesu alipowatibu
wakoma kumi aliwaambia waende wajioneshe kwa makuani. Bila shaka kabla ya
kuondoka walisema hatujapona aliwaambia nenda. Biblia inatwaambia walipokuwa
wanaenda wakapona. Utukufu ni mbele kwa mbele. Nelson Mendela alipofungwa Roben
Island miaka aliyokaa kwenye kisiwa hicho aliita miaka yenye giza. Lakini
utukufu ni mbele kwa mbele baada ya kukaa gerezani miaka 27 alikuwa Rais wa
Afrika ya Kusini. Baada ya miaka yenye giza alipata miaka yenye mwanga.
Watunzi wa
hadithi na filamu hutumia mbinu inayoitwa “ploti” ambapo mhusika mkuu hupata
matatizo makubwa na changamoto kubwa. Mwishowe hufanikiwa na hivyo kufanya
hadithi au filamu ivutie. Mungu ni Mtunzi wa watunzi ni Muumba wa watunzi.
Anapotengeneza hadithi ya maisha yetu anataka mwisho wa siku ivutie. Anaweza
kukupitisha kwenye matatizo makubwa mwisho wa siku utukufu ni mbele kwa mbele.
Yesu alipowaambia wafuasi wake kuwa atakufa msalabani jambo hilo lilisababisha
wingu zito la kukata tamaa katika maisha ya mitume. Aligeuka sura kuwakumbusha
mwisho wa mambo utakuwa huo. Petro aliposema kujenga vibanda vitatu bila kujua
ulikuwa ni utabiri wa kujenga Kanisa. Yesu alisema: “Wewe ndiwe Petro na juu ya
mwambao nitalijenga Kanisa langu wala milango ya kuzimu haitalishinda.” Baba wa
Kanisa Damas alikuwa na haya ya kusema: “Lakini Bwana hakukufanya uwe mjenzi wa
vibanda bali wa Kanisa la ulimwengu wote. Maneno yako yametimizwa na wafuasi
wako, kondoo wako kwa kujenga kibanda, si kwa ajili ya Kristo tu, bali kwa
ajili ya watumishi Wake. Lakini Petro hakusema hili kwa makusudi bali kwa kupitia ufunuo wa Roho Mtakatifu akifunua
mambo yatakayokuja.” Ukweli huu unabainisha umuhimu wa wazo letu, utukufu ni
mbele kwa mbele.
“Sijui kikomo
chako kitakuwa kipi, lakini neno moja najua: baadhi yenu watakaofurahi watakuwa
wale ambao wametafuta na kugundua umuhimu wa namna ya kutumikia,” alisema
Albert Schweitzer. Ili kupata furaha ya kugeuka sura ilibidi Petro na wenzake
washuke chini ili kuufanyia kazi utukufu wa mbele kwa mbele. Mtoto anapopelekwa
shule wazazi hawajui atakuwaje mbeleni utukufu ni mbele kwa mbele. Kuna mwalimu
wa shule ya awali aliyekuwa anawainamia watoto wadogo walipokuwa wanaingia
darasani. Alipoulizwa kwa nini alifanya hivyo alisema: “Hao watoto ni wabunge
wa kesho, ni maprofesa wa kesho, ni wafanyabiashara wa kesho.” Ni kweli utukufu
ni mbele kwa mbele.
No comments:
Post a Comment